Pin Song

Moni afunguka kuhusu tetesi za kujitenga na Roma


Msanii wa muziki wa hip hop, Moni Centrozone amedai hawezi kumtenga Roma Mkatoliki kutokana na matatizo yaliyotokea hivi karibuni.
Wawili hao mwezi uliopita wakiwa studio ya Tongwe Record walitekwa na watu wasiojulikana na baada ya siku tatu kuachiwa huku wakiwa na majeraha yaliyotokana na kuteswa.
Moni amejibu tetesi za watu wanaodai kwamba amejiweka mbali na msanii Roma tangu walipopata matatizo ya kutekwa na watu wasiojulikana kwa siku tatu kwa kujibu siyo kweli kwani wao ni zaidi ya marafiki hivyo ni vigumu kutengana.


“Roma ni damu yangu, ni kaka yangu ambapo kama siyo yeye nisingefika mapema kwenye ‘mainstream’ na maanisha ningechelewa kujulikana. Hata siku moja sijawi kufikiria kujitenga naye kwa sababu yeye kapata matatizo,” Moni alikiambia kipindi cha Enewz cha EATV. “Mimi nimetoa ngoma kwa sababu natakiwa kutoa na yeye bado anasubiri apone vizuri arudi kazini kwani bado tuna kazi nyingi za kufanya muda mfupi tuu baada ya kurejeshwa kwa studio ya Tongwe.”
Rapa huyo kwa sasa anafanya vizuri na wimbo ‘Tunaishi Nao’ alioutoa muda mfupi baada ya kurejea uraiani tangu alipotekwa na watu wasiojulikana akiwepo yeye, Roma na Prodyuza Bin Laden na msaidizi wa ndani.
Jeshi la polisi halijatoa taarifa yoyote kuhusiana na uchunguzi wa tukio hilo.